EAST AFRICA YOUTH TANZANIA

EAST AFRICA YOUTH TANZANIA

Thursday, December 8, 2016

Afrika ijifunze kutoka Korea

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Afrika ijifunze kutoka Korea, Mawaziri.
Nchi za Afrika zimehimizana kutumia sera , mbinu na mfumo wa maendeleo uliotumiwa na Jamhuri ya Korea kufanya mapinduzi makubwa ya uchumi, viwanda na teknolojia katika kipindi cha miongo michache iliyopita.
Hayo yamejiri kwenye Mkutano wa  Mawaziri wa  nchi za Afrika na Korea uliohitimishwa leo jijini Addis Ababa, Ethiopia.
"Katika miaka ya 1960 hali ya uchumi na mazingira ya Korea yalikuwa yanalingana na bara la Afrika, hivyo, mfumo ulioifanya Korea kufanya mapinduzi ya uchumi unafaa kutumiwa na bara la Afrika kwa kuwa mazingira yetu yanafanana".
Katika mkutano huo ambaoTanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga, Mawaziri walielezea kuridhishwa na ushirikiano huo tokea ulipoanzishwa mwaka 2006, kwa kuwa unazingatia maslahi ya pande zote na haufungamani na masharti ya aina yoyote.
Walisema kuwa Bara la Afrika lina fursa lukuki zikiwemo maliasiri kama madini, mafuta na ardhi nzuri kwa kilimo.
 Rasilimali hizo miaka yote zimekuwa zikiuzwa nje bila kuendelezwa kutokana na ukosefu wa viwanda na teknolojia, hali iliyochangia  kwa kiasi kikubwa kulifanya bara hilo kubaki nyuma kimaendeleo.
Hivyo, kupitia jukwaa hilo la ushirikiano na Korea, bara la Afrika litapokea misaada ya fedha za maendeleo na teknolojia  itakayotumiwa kujenga viwanda vya kusindika rasilimali ili kuziongezea thamani.
Kwa kuwa maendeleo na amani na usalama ni vitu vinavyotegemeana, Mawaziri walisisitiza umuhimu wa kutunza amani barani Afrika kwa kushirikiana na Korea.
 Walibainisha masuala mbalimbali yanayotishia amani ya  dunia likiwemo tatizo la ugaidi wa kimataifa. Walikubaliana kuwa ugaidi ni changamoto ya ulimwengu mzima na ili ufumbuzi wake upatikane lazima wadau duniani kote washirikiane.
Ushirikiano wa nchi za Afrika na Korea unatimiza miaka 10 mwaka huu tokea ulipoanzishwa mwaka 2006. Kwa muktadha huo, ulisisitizwa umuhimu wa kufanya tathmini na ufuatiliaji wa miradi ya utekelezaji ili kubaini mafanikio mapungufu na changamoto.  Hiyo itasaidia kuchukua hatua stahiki katika kufikia malengo yaliyowekwa na umoja huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se alieleza mafanikio ya ushirikiano huo tokea kunzishwa kwake. Alisema katika eneo la ushirikiano wa kiuchumi na Afrika, Korea ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa tano wa Mawaziri wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea na Afrika mwezi Oktoba 2016.
 Katika mkutano huo, Korea iliahidi kutoa Dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya kusaidia masuala ya kiuchumi barani Afrika. Fedha hizo zinatarajiwa kuongezeka  mara dufu katika kipindi kijacho. Aidha, Korea inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la ushirikiano wa viwanda kati ya Korea na Afrika katika wiki mbili zijazo.
Vile vile, Korea imeongeza mara dufu misaada ya maendeleo kwa bara la Afrika na ile misaada ya maendeleo inayohusisha nchi mbili (bilateral)  itaongezeka kutoka asilimia 24 hadi kufikia asilimia 35 itakapofika mwaka 2020.
Waheshimiwa Mawaziri walihitimisha mkutano wao kwa kuridhia nyaraka mbili ambazo ni Tamko la Addis Ababa na Mwongozo wa Ushirikiano kati ya Korea na Afrika. Mwongozo huo umeainisha miradi mbali mbali itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano 2017 - 2021. Maeneo hayo ni pamoja na: biashara, kuendeleza viwanda na uwekezaji; uzalishaji katika kilimo na kiwango cha mavuno; uchumi wa bahari, uendeshaji wa bandari na usafiri wa majini; kuwaendeleza vijana na kuwajengea uwezo wanawake.
Wajumbe walikubaliana kuwa mkutano ujao utafanyika Seoul, Korea mwaka 2021.
Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI.
TAREHE 08 DESEMBA 2016 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisoma hotuba ya Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Ushirikiano wa nchi za Afrika na Jamhuri ya Korea uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba 2016.
Mhe. Waziri Mahiga akipitia makabrasha ya mkutano. Nyuma ya Mhe. Waziri ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na kwenye Umoja wa Afrika, Mhe. Naimi Aziz na Afisa wa Ubalozi huo, Bi Suma Mwakyusa.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje nao wakifuatilia mkutano huo. Kutoka kushoto ni Bw. Gerlad Mbwafu, Katibu wa Waziri, Bi. Berther Makilagi, Afisa Dawati la Korea na Bw. Benedict Msuya anayemwakilishsa Mkurugenzi wa Asia na Australasia.

Picha ya pamoja
 

No comments:

Post a Comment